FIKRA ZANGU
BARUA KWA WAVUMBUZI 30/09/2023
✍️ Peter Philemon
Nawasalimu enyi wanadamu mliojaliwa upeo mkubwa sana na mlioweza kushinda changamoto nyingi za mioyo yenu.
Huu ni mwaka 2023 mwezi wa 9 tarehe 30, pengine mnajiuliza kuwa ingekuwa vyema nisubiri ifike tarehe 1 ya mwezi mpya ambayo ni kesho tu, sababu kubwa ni kuwa mambo mapya kwenu hayana nafasi tena, mmeuishi uzamani na bado mtaendelea kuwa katika uzamani, Dunia ya sasa ni mpya kwenu na imewaacha mno hasa katika kufikiri.
Dunia ya sasa wavumbuzi wapya wanauishi mtazamo wenu na hesabu zenu, wanawasifia katika kile mlichokianza kwa ukubwa kwa wakati wenu, ila Kwa sasa ule ukubwa wa fikra zenu unaonekana ni fikra finyu tu mbele ya sayansi mpya iliyojengwa mara 1000 zaidi ya wakati wenu.
Unakumbuka barua yako uliyomtumia baba yako Mzee Bell mwaka 1876 ewe Alexander Graham Bell? Usijichoshe kufikiri binafsi naikumbuka sana!! Pengine unajiuliza inawezekanaje mtoto mdogo tu mimi kukumbuka ulichoandika miaka 147 Kwa wakati wangu huu? Baada ya kifo chako tarehe 2 wa nane 1922, familia yako ilipeleka vyote ulivyowahi kuvihifadhi katika maandishi huko jumba la Makumbusho, sasa barua yako ni sehemu ya Makumbusho tena yenye kupewa heshima kubwa.
Ulimuandikia baba yako kuwa wakati unakuja ambapo haitamlazimu tena mtu kwenda nyumbani kwa mwingine kwa ajili ya mazungumzo, bali simu ndizo zitakazokuwa daraja la kuwaunganisha. Baba yako alikuona mwendawazimu hadi pale ulipofanikisha uundaji wa simu yako ya kwanza na Dunia ikauheshimu ubunifu wako, ukawa mwanadamu wa kwanza kuvumbua simu kwa kuthibitisha ufanyaji kazi wake ulijifungia chumbani na msaidizi wako bwana Watson alikuwa chumba kingine na ukampigia simu na kumwambia "bwana Watson, njoo hapa, nakuhitaji" Je unatambua maneno haya uliyoyazungumza yametumika kama wimbo wa kupitia kwenye simu za mkononi zilizotengenezwa Karne ya 20? Yote haya ni kukuenzi kwa uvumbuzi wako.
Ukipata wasaa bwana Alexander, tafadhali nisalimie Emile Berliner, ugunduzi wake wa microphone 🎤 umeisaidia Dunia Kwa kiasi kikubwa, wewe uliona ugunduzi wake ukaubariki kupitia kushiriki nae katika kutengeneza Mic za simu yako ya kwanza, Leo katika mikutano sauti hubadilishwa kuwa umeme kupitia ugunduzi wake, pia hata lile wazo lake la kutengeneza kifaa kitakachocheza mziki alichokiita gramofoni na akaliweka wazo lake katika vitendo, limezalisha uwepo wa kaseti, mp3 na card reader ambazo Kwa sasa zinaonekana zimepitwa na wakati.
Tarehe 2 mwezi wa nane 1922 Dunia ilirekodi kifo chako, Kwa heshima uliyoipatia Dunia kupitia uvumbuzi wako wa thamani ambao umepelekea uwepo wa simu janja, vishikwambi na simu za mkononi, nchi ya Marekani iliamua kuzima huduma zote za simu kwa dakika moja wakati wa mazishi yako. Najua unaisoma barua hii mwaka 1921 mwaka mmoja kabla ya kifo chako, tafadhali jisikie mwenye Imani na Dunia yetu kupitia kazi zako, kama utaazimia usafiri katika wakati kama alivyotuaminisha kijana uliempenda sana Albert Einstein, tafadhali usije ukajifanya mjuaji nitakufundisha jinsi ya kutumia simu ili usiaibike. Asante tafadhali mpatie msafiri wakati aliekupatia barua hii usigeuze nyuma ya barua huku ni kwa wengine.
Nakuandikia Nikola Tesla, mvumbuzi wa umeme wa mkondo geu (Alternating Current), binafsi nikupongeze Kwa kuwa na moyo wa chuma hasa pale ambapo Thomas Edison mvumbuzi wa mkondo nyofu wa umeme (Direct Current) alipoamua kukuharibia soko la uvumbuzi wako Kwa kudai kuwa umeme wako sio salama kwa matumizi. Najua unamchukia sana Thomas ila nakusihi msamehe tu kwasababu Dunia yetu kwa sasa inatumia uvumbuzi wenu kwa pamoja katika matumizi ya kila siku, jambo hili litakushangaza sana ila msamehe Thomas nakusihi.
Nikupongeze kwa uundaji wa mashine inayofua umeme wa Maji, japokuwa ilikuwa ni mwaka 1896, ila huwezi kuamini kwamba karibia nchi zote za Afrika bado zinatumia mashine zako zilizoboreshwa sana. Jina lako limebaki kuwa juu sana kwani tajiri wa Dunia Kwa sasa Elon Musk anamiliki kampuni yenye jina lako (Tesla Company), na tena anatengeza magari yanayotumia umeme kama ulivyokuwa ukiota hapo zamani, wazo lako la kucheza matukio kupitia kifaa kitakachotumia umeme lilifanyiwa kazi mwaka 1936 na John Lorgie ambae tunamfahamu kama mvumbuzi wa kwanza wa runinga au Television 📺 katika lugha yako. Kama utajumuika na Alexander kunitembelea tafadhali kuwa makini Kuna uzalishwaji wa umeme kupitia uranium kipindi hichi. Tafadhali usigeuze upande wa nyuma wa barua hii huko ni kwa Karl Benz, miaka 30 nyuma ya mwaka wako wa sasa, mpe barua hii msafiri wakati, Asante.
Nakuandikia ewe Karl Benz, mwanaume shupavu na mvumbuzi mwenye kuheshimika sana, hivi unafahamu kuwa Mercedes Benz ni gari la anasa katika Dunia yangu kwa sasa? utashangaa kwanini jina la baba yako Mzee Benz lipo mbele ya Mercedes, najua upo kwenye kampuni yako ya Motor wagen, unawaza sana jinsi gani utafahamika sana Duniani Kwa wakati wako, usife moyo gari lako la matairi matatu uliloliita Motor Wagen jina la kampuni yako ndilo gari la kwanza ulimwenguni na wewe ndio mvumbuzi wa kwanza wa magari, ila kitakachokusikitisha ni kuwa watoto wako wameshindwa kusimamia biashara yako na ipo chini ya watu wengine wenye ujuzi na weledi kuliko hata watu wa wakati wako.
Wanazalisha magri ya kifahari sana kupitia jina lako, watu wengi wanayatamani na kuweka mipango ya kuyamiliki. Kama utaazimia kusafiri katika wakati nakukaribisha ila usiwe mjanja sana maana hata Mimi sijui Benzi inawashwa vipi!! Ila nitakupeleka Kwa meneja wa kampuni yako ukajifunzie hapo maana mambo yamebadilika sana. Nikuache uendelee na ujenzi wa kampuni yako tafadhali mpatie barua hii msafiri wakati maana yanayofuata ni ya miaka 6 nyuma ya mwaka wako wa sasa. Asante
Nakuandikia ewe Scotty ulierekodi Kwa utani sauti ya mwimbaji alieimba wimbo wa 'mwanga wa mwezi' wimbo pendwa wa wakati wenu Scotty, hivi unafahamu kile kifaa ulichorekodia wimbo huo mwaka 1860 Aprili 4 ndo kifaa kilichohifadhiwa wakati wetu chenye kumbukumbu ya nyimbo ya kwanza duniani kurekodiwa? Jipongeze Scotty wewe ni mwanadamu wa kwanza kurekodi wimbo. Kwa sasa zaidi ya nyimbo milioni na zaidi zinarekodiwa studio na kuchezwa na vyombo vingi vya muziki, unapoadhimia kusafiri kuyashuhudia haya usijidai una akili kunizidi maana utakuwa mwanafunzi wa kila utakachokiona, pia usisahau kumsalimia Louis Le Prince rafiki yako kipenzi utakaekutana nae miaka 20 mbele ya wakati wako umsihi aendelee na bidii utakapokutana nae kwani kwenye Dunia yetu kwa sasa yeye ndie mwanadamu wa kwanza kuongoza uzalishwaji wa sinema, atakapoyafikia mafanikio hayo umpongeze kwani kazi yake hiyo imetoa ajira kubwa Kwa watu wa Dunia hii. Nikutakie siku njema na bidii njema Scotty, msihi msafiri wakati arudi upesi maana Kuna Mengi ya kuwaandikia wengine. Asante sana.....
Mimi ni wenu Peter Philemon mwandishi na mnajimu anaeziishi falsafa wezeshi katika ulimwengu huu mpya uliojaa sayansi na teknolojia za kila aina.
🥇Bravo!!!! Tukutane Makala zijazo.....✍️ Peter Philemon
MAFANIKIO NI ZAO LA NDOTO
Karibu katika usomaji wa makala hii!!!
✍️ Peter Philemon
🥇 Wewe ni nguzo muhimu sana si tu kwenye Maisha yako binafsi pia Kwa wengine waliokuzunguka.
Kila mmoja ana mawazo tofauti tofauti, utofauti huo ni wa kipekee sana na uzoefu wake huchagizwa na ndoto zisizokoma akilini, ndoto ni mawazo yanayozunguka akilini mwako ila hayajakamilishwa katika utekelezaji unaokusudiwa. Hivyo si Vibaya kuishi katika ndoto kama utakusudia utekelezaji wake kupitia mipango yako ya muda mfupi na Ile ya muda mrefu.
Kama mtu anaesafiri katika bahari kama Columbus mvumbuzi wa pwani ya Amerika, ndivyo mjumuisho wa mambo yanayoijia akili kupitia ndoto, wapi unaenda? Unataka Nini? Kwanini unasafiri? Columbus alijibu "Natazamia kwenda mahali nisipopajua nasafiri kama niko ndotoni, ninachotaka ni kuifikia pwani safi na yenye udongo wenye rutuba isiyoelezeka, yenye watu wakarimu na wastaarabu watakaonipokea kama mgeni wao Kwa amani, ninasafiri Kwa ajili ya nchi yangu na safari ni Maisha yangu". Christopher Columbus mvumbuzi wa pwani ya Amerika.
Msanii mdogo huwa na kawaida ya kutazamia kufanana na msanii mkubwa sana na mwenye hadhi zaidi ya kawaida aliyonayo chipukizi katika fani ya sanaa, hii ni ndoto, uamuzi na uchaguzi ni nguzo za kufanikisha ndoto kuwa halisi, ni katika kujaribu na kushindwa, kuaibika na kuaibishwa, kama kikwazo Kwa yeyote anaetazamia mafanikio. Ustahimilivu wa msanii huyu mdogo ndio utakaomfikisha kwenye ndoto anayeiota ili aiishi. Mtaalamu wa Programu za Kompyuta daima huishi katika kuzijaribu Programu na kuzipangilia ili ziwe na ufanisi unaokusudiwa, kama hatua zilivyo katika ukuaji, ufanisi wa mipango yako hutegemea majaribio na mipangilio, usiogope kujaribu kama utakuwa na kusudi za kuishi ndoto zako siku za usoni. "Nitahakikisha kabla sijaingia kaburini nitayaishi Maisha katika upana wake kulingana na urefu wa Maisha yangu" alisikika mhenga mmoja. Maisha huwa na upana licha ya urefu wake pia, kuishi upana wake ni kuyafurahia matunda yake mazuri katika ustaarabu na weledi. Kusudio huwa ni chachu ya kufanikisha lolote.
Mhandisi huthibitika zaidi na kile anachokifanyia kazi katika kuonekana, ubora wa matokeo ya kazi zake humpa hadhi mhandisi, licha ya mahangaiko makubwa kupitia kulala Kwa masaa machache tu lakini haishii tu kuota usanifu wake ila ana nyenzo za kukamilisha kazi yake ili iwe bora zaidi. Huwezi kuziishi ndoto pasipo kutayarisha mazingira bora yanayoanza na ufahamu wa kina kuhusu kusudi lako.
Una uhakika kweli itaruka? ni swali aliloulizwa mtaalamu wa mwanzo kabisa aliepeleka model ya ndege ndogo kupitia mchoro aliouandaa Kwa muda wa miaka kadhaa, alitaka kuleta mapinduzi makubwa katika teknolojia ila Kwa wataalamu wengine walionyesha kuwa na mashaka nae, mradi wa mabilioni ya fedha katika karatasi ya mtaalamu mmoja mwenye Imani. Kilichofuata ni zaidi ya matokeo ya urukaji, faida juu ya faida, ukuaji wa biashara na uokoaji wa muda kupitia kwenye karatasi iliyochorwa na mtaalamu huyo mwenye Imani. Leo Kuna mashirika Mengi ya ndege duniani, mafanikio na uthibitishwaji wa Imani ya mtaalamu huyu umeipa hadhi sayari hii ya Dunia.
Daima Imani huwa nguzo muhimu ya kuifanya ndoto unayoikusudia kuwa halisi, Imani ni kiongozi bora wa saikolojia ya mwanadamu tangu kuumbwa kwake, jijengee kawaida ya kuwa na Imani hata katika mambo yako madogo huo ndio uhai wako katika chochote unachokifanya.
"Naamini nazungumza na kamanda wa Jeshi la Navy, naagiza urushwaji wa kombora mbili zenye uzito mkubwa ndani ya Jiji ya Pyeongyang, hii ni amri" ni sauti ya Raisi Richard wa Marekani akimuagiza kamanda wake kutekeleza amri yake ya kuuteketeza mji mkuu wa Korea kaskazini. Alfajiri baada ya usiku huo kamanda akawasiliana na Raisi akimuuliza ni kweli atekeleze amri hiyo, Raisi alishtuka na akamueleza kuwa alikuwa amelewa na hakutarajia kama atatoa amri hiyo. Kutokukurupuka Kwa kamanda katika utekelezaji kuliiweka salama Korea kaskazini hivyo hivyo katika Maisha subiri mpaka fursa ijikamilishe katika kutumiwa usikurupuke, huku ndiko kuishinda nafsi.
Ni hayo tu Kwa Leo tukutane katika Makala zijazo.